Kwa wale watu wanaofahamu vyema historia ya Uislamu, mwezi wa Muharram hukumbusha mapambano makubwa ambayo yalifanywa na Imam Hussein (as) kwa ajili ya kurekebisha na kuhuisha dini ya babu yake Mtume Muhammad (saw) ambayo ilikuwa imepotoshwa kwa kiwango kikubwa na maadui wa Uislamu pamoja na watu waliokuwa na tamaa ya kuitawala dini kifalme. Kwa ibara nyingine ni kuwa mwezi wa Muharamm umefungamana kikamilifu na jina la Imam Hussein kwa kadiri kwamba kutajwa mwezi huo ni sawa na kutajwa jina la imam huyo mtoharifu. Huyo ni mtukufu ambaye aliuawa shahidi akiwa na wafuasi wake wachache 72 katika ardhi ya Karbala mwaka wa 61 Hijiria. Tukio hilo muhimu katika historia ya Uislamu lilidhihirisha wazi thamani kubwa za kimaadili, ushujaa na kujitolea kwa Imam Hussein na wafuasi wake wachache mbele ya hujuma kubwa na ya kinyama ya maadui wake. Sifa maalumu za mapambano ya Imam Hussein ni kuwa thamani za mapambano hayo hazikubaki kwenye mmbano wa zama na sehemu yalikotokea, bali zilizweza kuvuka mipaka ya kijiografia na historia na kuweza kuathiri mataifa mbalimbali katika zama zote za historia ya mwanadamu. Hii leo kila mara watu wanapozungumzia mapambano dhidi ya dhulma na uaonevu na umuhimu wa kutetea haki na uadilifu jina la Imam Hussein bin Ali (as) hudhihiri na kuzungumzwa na kila mtu anayefahamu vyema thamani za mapambano dhidi ya dhulma. Je, ni mapambano mangapi yaliyotokea katika historia ya mwanadamu na waanzilishi pamoja na viongozi wa mapambano hayo kusahaulika, lakini ya mapambao ya Imam Hussein tokea yalipotokea hadi leo yangali yanang'ara kama jua na miale yake angavu na yenye joto kuangaza kwenye giza totoro na kuzipa joto na uchangafu nyoyo zilizochoshwa na dhulma? Salamu kwa Imam Hussein (as), salamu kwa hakika ambayo daima i hai, salamu za Mwenyezi Mungu kwa yule ambaye alitoa roho yake kwa ajili ya kuhuisha dini ya Allah ili kupeperusha daima bendera ya mwongozo wa Kiislamu.
Moja ya majukumu muhimu ya kiongozi wa Kiislamu ni kuwaweka watu kwenye njia nyoofu ya wongofu. Moja ya mambo yaliyomfanya Imam Hussein (as) kusimamisha mapambano katika zama zake ni kupotea watala na jamii kutoka kwenye misingi na mafundisho ya dini. Huo ni ukweli mchungu ambao taratibu ulidhihiri katika kipindi cha miaka 50 baada ya kuaga dunia Mtume (saw). Kupuuzwa na kusahaulika kwa wasia wa Mtume na kutengwa Watu wa Nyumba yake (as), kudhoofika thamani za kimaanawi katika jamii, urundikaji mali wa watawala na kuenezwa bidaa, uzushi na upotofu katika jamii, yote hayo ni mambo yaliyoandaa mazingira ya jamii hiyo kurejea taratibu katika zama za ujahili. Mwenendo huo wa mporomoko wa maadili na mafundisho ya Kiislamu uliendelea hadi kufikia kipindi ambacho jamii ya Kiislamu ilitawaliwa na mtawala dhalimu na fasiki kama Yazid bin Muawiyya, jambo lililotoa pigo kubwa kwa umma wa Kiislamu. Mara tu baada ya kuchukua madaraka kutoka kwa baba yake Muawiyya, Yazid alimtaka mjukuu wa Mtume Imam Hussein (as) kumbai na kutangaza utiifu wake kwake. Jambo hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa kwake kwa kutilia maanani nafasi ya juu aliyokuwa nayo Imam Hussein (as) katika umma wa Kiislamu. Yazid alikuwa ni mtu ambaye hakufaa hata kidogo kutawala umma wa Kiislamu na watu wote wakitambua vyema kiwango chake cha juu cha ufuska, uchafu, ulevi na utovu wa maadili. Kwa msingi huo ni wazi kuwa mtu kama Imam Hussein (as) kamwe hangekubali kumpa Yazid mkono wa beia na utiifu. Kwa mtazamo wa Imam Hussein (as), Bani Umaiyya ni watu ambao walikuwa wameachana na misingi ya dini ya Mwenyezi Mungu na kusisitiza juu ya kuendelea na tabia zao za ufuska na ufisadi katika jamii ya Kiislamu. Hatua ya Imam kukataa kumbai Yazid ilikuwa ni ishara ya wazi kwamba mtawala huyo dhalimu na fasidi hakufaa hata kidogo kuingoza jamii ya Kiislamu. Kufuatia hatua hiyo, mtawala wa Madina alipewa amri na Yazid ya kubana na kufanya maisha ya Imam Hussein (as) kuwa magumu. Kutokana na hali hiyo Imam aliamua kuuhama mji wa Madina ili kutafuta sehemu nyingine bora zaidi ya kuwaongoza watu na kuwabainishia hali halisi ya mambo ya umma wa Kiislamu. Katika zama hizo, mji mtakatifu wa Makka ulikuwa sehemu bora zaidi ya kuendeshea shughuli hiyo ya mapambano na mwongozo, na hasa ikitiliwa maanani kwamba msimu wa hija ulikuwa unawadia ambapo umati mkubwa ungekusanyika katika mji huo kwa ajili ya ibada. Alipokuwa akiondoka mjini Madina Imam Hussein (as) alisema: "Mimi ninaondoka mjini Madina kwa ajili ya kurekebisha na kuhuisha umma wa babu yangu, na ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu." Baada ya kuwasili mjini Makka, Imam Hussein (as) alifanya juhudi kubwa za kuandaa mazingira ya mapambano dhidi ya Yazid.
Katika upande wa pili, wapenzi wa Ahlul Beit wa Mtume (saw) kutoka mji wa Kufa katika Iraq ya hivi sasa, waliposikia kwamba Imam amekataa kumbai Yazid, walifurahia sana jambo hilo kwa sababu walikuwa wamechoshwa na dhulma ya Bani Umaiyya. Baadhi ya wakuu wa Kufa ambao walikuwa waungaji mkono wa Ahlul Beit (as) walimtumia barua Imam Hussein (as) wakimtaka aende katika mji huo. Katika barua hizo walitangaza wazi kwamba walikuwa tayari kushirikiana kwa kila njia na Imam katika kufanikisha malengo yake. Baada ya kupata barua hizo, Imam Hussein (as) alimtuma Muslim bin Aqil mjini Kufa ili aende kuchunguza zaidi hali ya mambo huko. Historia inatwambia kwamba maelfu ya watu walitangaza utiifu wao kwa Muslim bin Aqil kwa niaba ya Imam Hussein (as). Baada ya kuchunguza na kutathmini hali ya mambo, Imam Hussein aliamua kukatiza ibada yake ya hija na kuondoka mjini Makka tarehe 8 Dhul Hijja mwaka 61 ili kuelekea Kufa. Lakini alipokuwa njia kuelekea huko habari zilimfikia Imam kwamba hali ya mambo mjini humo ilikuwa imebadilika na kwamba Yazid alikuwa amemuuzulu gavana wa Kufa na kumuweka mahala pake Ubeidullah bin Ziad, mtawala fasidi, dhalimu na katili kupindukia. Ibn Ziad alizima sauti ya malalamiko ya watu wa Kufa kwa kutumia ukatili na unyanyasaji wa hali ya juu. Baadhi ya watu hao walikengeuka na kutomuunga mkono tena Imam Hussein kutokana na woga, mateso au hongo waliyopata kutoka kwa dhalimu huyo. Watu walioamua kuendelea kumuunga mkono Imam Hussein (as) ima waliuawa shahidi au kufungwa kwenye jela za kuogofya. Muslim bin Aqil, mjumbe wa Imam Hussein (as) pia aliuawa shahidi katika matukio hayo. Licha ya kupata habari hiyo ya kuhuzunisha, Imam aliamua kuendelea na safari yake lakini baada ya kuwakamilishia hoja na kuwabainishia vyema wafuasi wake hatari ya kifo iliyowasubiri huko mbele. Aliwaambia: "Enyi watu! Watu wa Kufa wametukimbia. Kila mmoja wenu anayetaka kurejea anaweza kufanya hivyo hivi sasa." Historia inasema kwamba kuna watu walioondoka kwenye msafara huo wa Imam Hussein mahala hapo na kumuacha Imam akiwa na idadi ndogo tu ya wafuasi wake waaminifu, ambao alifuatana nao kuelekea Kufa. Moyo na azma ya Imam Hussein ya kupambana na dhulma ilikuwa kubwa na imara kiasi kwamba hakuogopa wala kuchelea chochote hata baada ya kuachwa na idadi ndogo tu ya wafuasi. Hii ni kwa sababu alisikia kutoka kwa baba yake maneno yafuatayo yenye umuhimu na thamani kubwa: 'Mkiwa kwenye njia ya wongofu, msihofu kutokana na uchache wa wafuasi wa njia hiyo."
Imam Hussein (as) alikuwa akielewa vyema kwamba hangeweza kushinda kijeshi umati mkubwa wa maadui wake waliokuwa wamejizatiti vyema kwa silaka kwa kutegemea wafuasi wachache aliokuwa nao wala hakutegemea kupata ushirikiano na uungaji mkono wa watu waliokuwa na imani dhaifu na waoga kupindukia. Jambo lililokuwa na umuhimu kwa imam huyo ni utekelezaji wa majukumu yake ya kidini bila kujali matokeo yake. Alikuwa akiwaza tu juu ya udharura wa kutekelezwa majukumu aliyopewa na Mwenyezi Mungu hata kama jambo hilo lingepelekea auawe shahidi. Ushindi na kushindwa ni mambo yaliyokuwa na maana tofauti kabisa katika mantiki ya Imam Hussein (as). Msafara wa Imam Hussein (as) haukuwa umefika katika mji wa Kufa kabla ya kuzingirwa na jeshi la askari 30,000 la Yazid katika jangwa la Karbalaa. Kukabiliana kwa watu wachache wenye imani thabiti kwa upande mmoja na jeshi kubwa lenye imani dhaifu kwa upande wa pili katika siku ya Ashura mwaka 61 Hijiria kulidhihirisha tukio muhimu na lisilo na mfano wake katika historia ya mwanadamu. Mapambano ya Imam Hussein (as) yalikuwa dhihirisho halisi la kimaadili na kiutu. Hii ni kwa sababu medani ya vita katika siku hiyo ulikuwa ni uwanja wa kukabiliana imani na umaanawi na kufri na ufisadi. Hii ni kwa sababu katika siku hiyo watu wenye imani thabiti hawakutarajiwa ila kuonyesha hamasa na thamani za kiutu. Ni kutokana na ukweli huo ndipo harakati yenye thamani kubwa ya mwamko ya Imam Hussein (as) ikadhibitiwa na kubaki milele katika historia ya mwanadamu na kunukuliwa kutoka kizazi hadi kizazi kingine hali leo hii.
Source: www.kiswahili.irib.ir
No comments:
Post a Comment