Mfalme wa Qatar, Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani amefanya ziara ya siri ya kuutembelea utawala wa Kizayuni licha ya uhakika kwamba Qatar haina uhusiano wa kisiasa na Israel.
Mkanda mmoja wa video unamuonesha Amir huyo wa Qatar pamoja na Waziri Mkuu wake Sheikh Hamad bin Jasim bin Jabir Aal Thani wakikaribishwa na Tzipi Livni, mkuu wa chama cha Kadima cha Israel.
Mfalme huyo wa Qatar ameonana pia na maafisa wengine kadhaa wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kuwekwa mkataba mpya wa gesi kati ya Doha na Tel Aviv ni miongoni mwa masuala muhimu yaliyojadiliwa katika ziara hiyo ya Amir wa Qatar na ujumbe wake mzito huko Israel.
Qatar imeweka mkataba mpya wa gesi na Israel baada ya mkataba wa gesi kati ya utawala wa Kizayuni na Misri uliokuwa umewekwa wakati wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak kuingia hatarini kufuatia wanaharakati wa Kiislamu kupata ushindi mutlaki katika uchaguzi wa hivi karibuni wa Bunge nchini Misri na ambao ulikuwa wa kwanza tangu kupinduliwa kibaraka mkubwa wa nchi za Magharibi, Hosni Mubarak.