Mshambuliaji machachari wa klabu ya Real Madrid ya Uhispania na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Christiano Ronaldo ametoa kitita cha euro milioni moja na nusu kwa ajili ya ukarabati wa shule zilizoharibiwa vibaya na mashambulizi ya mabomu ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza. Hii si mara ya kwanza kwa Christiano Ronaldo kutoa misaada kwa wananchi wa Gaza, kwani mwaka jana pia alinadisha viatu vyake vya michezo na fedha zilizopatikana alizikabidhi kwenye taasisi ya Real Madrid kwa shabaha ya kusaidia shule za Gaza. Hadi sasa Taasisi ya Real Madrid imeweza kujenga shule 167 katika nchi 66 duniani. Ronaldo alikuwa mchezaji ghali mno duniani katika historia ya mchezo wa kabumbu baada ya kuhama klabu yake ya zamani ya Manchester United ya Uingereza na kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa euro milioni 93.9.
Source: kiswahili.irib.ir