Waziri wa Elimu, Teknolojia na Utafiti wa Iran Kamran Daneshjoo ametangaza kwamba zaidi ya wanafunzi 1000 wameomba kubadilisha taaluma zao kuelekea taaluma ya Fizikia na Uhandisi wa Nishati ya Nyuklia.
Daneshjoo amesema, wanafunzi wapatao 300 wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha Sharif na vilevile wanafunzi zaidi ya elfu moja wa muhula wa kwanza wa masomo katika vyuo vikuu nchini wameomba kubadilisha taaluma zao ili kusomea fani ya Fizikia na Uhandisi wa Nishati ya Nyuklia.
Amesema jambo hili linaashiria kwamba mbinu za mauaji zinazofanywa na maadui dhidi ya wasomi wa Nyuklia wa Iran hazina taathira yoyote ya kuwatia woga wanafunzi hao, na kwamba mbinu hizo hazikuwasaidia lolote maadui hao.
Ameashiria kwamba kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na mtandao wa Kielimu wa Kimataifa "Escobos" Iran imejipatia nafasi ya kwanza katika upande wa elimu, wakati ambao ilikuwa ya pili baada ya Uturuki.
Waziri huyo ameongeza kwamba idadi ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu imefikia milioni nne huku idadi ya waliochaguliwa ikizidi pia, na amesema kwamba wakuu wa vyombo vya usalama wanafanya juhudi kubwa usiku na mchana katika kuhakikisha maisha ya wanafunzi hao yanakuwa salama kutokana na njama mbaya za maadui.